NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA MHE. KIPANGA JUMA OMARY (MB) ATEMBELEA MAMLAKA YA ELIMU TANZANIA

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga  (Mb) amewataka watendaji wa taasisi za serikali ikiwemo Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kufanya kazi kwa bidii na kuongeza tija katika uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza kwenye Mamlaka ya Elimu Tanzania, (TEA) Mhe. Kipanga amesema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha malengo ya elimu yanayoratibiwa kitaifa na Serikali ya Awamu ya tano yanatekelezwa kwa ufanisi.

"Nimekuja kwenu watumishi wenzangu ili niweze kujua utendaji wenu wa kazi unavyokwenda nijue chakujifunza ili kiweze kunisaidia katika kutoa majibu ya Serikali Bungeni", Alisema Kipanga.

Aidha Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli imejidhatiti katika kuhakikisha mazingira ya Utoaji wa elimu kwa watoto wa Kitanzania yanaendelea kuboreshwa siku Hadi siku hivyo ni vyema watumishi wa serikali na taasisi binafsi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa wenye tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye amesema taasisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kulingana na mipango na sera za kitaifa na ilani ya Chama cha Mapinduzi kama sehemu ya kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea Watanzania wote Maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa fedha na Utawala (TEA) Erasmus Kipesha amebainisha kuwa ziara ya Naibu Waziri Elimu Sayansi na Teknolojia katika Taasisi hiyo itaongeza chachu kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa nguvu zote.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia kwenye Mamlaka ya Elimu Tanzania ni ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwezi Desemba mwaka 2020.