KONGAMANO LA WADAU NA WACHANGIAJI WA MFUKO WA ELIMU 2021

 

DAR ES SALAAM                                                                                        23 JUNI 2021

 

KONGAMANO LA WADAU NA WACHANGIAJI WA MFUKO WA ELIMU 2021

 

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeandaa Kongamano la siku moja la wadau na wachangiaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa litakalofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 24 Juni 2021.

 

Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo lenye kauli mbiu, Changia Mfuko wa Elimu; Boresha Miundombinu ya Elimu ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce L. Ndalichako (MB) ambaye pia katika shughuli hiyo atatoa vyeti vya utambuzi wa wachangiaji wa Mfuko wa Elimu kwa mwaka 2019/2020.

 

Shughuli  zitakazoambatana na Kongamano hilo litakaloshirikisha wadau zaidi ya 200 ni pamoja na kuonyesha miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mfuko wa Elimu na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi; na majadiliano juu ya michango ya wadau kwa maendeleo ya miundombinu ya elimu nchini.

 

Jukumu la msingi la Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibwia na TEA ni kuongeza jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Kupitia Mfuko huu taasisi za elimu kuanzia ngazi ya shule za Msingi, shule za Sekondari, vyuo vya kati na vyuo vya Elimu ya Juu vinapata fursa ya kufadhiliwa miradi inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia.

 

Zaidi ya Shilingi Bilioni 9.1 zilitumika kufadhili miradi 96 ya elimu katika Shule 88 na Taasisi moja ya Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

 

Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shule 116 zinanufaika na miradi 123 inayogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 9.4.