WAZIRI WA ELIMU, SANYANSI NA TEKNOLOJIA, PROF. ADOLF MKENDA AVUTIWA NA WANUFAIKA WA SDF

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, leo tarehe 13 Juni, 2022  amekutana na kuzungumza na  baadhi ya wanufaika wa mafunzo ya kuendeleza ujuzi yanayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ambao  ni utekelezaji wa Mkakati wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitia  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwezesha watanzania kupata mafunzo ya ujuzi  yanayohitajika katika soko la ajira. Mafunzo hayo yanafadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Dunia (WB) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Prof. Mkenda amekutana na  baadhi ya washiriki hao, alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ni mratibu wa Mfuko wa SDF  katika maonyesho ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayofikia kilele, leo katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.

Akiwa katika banda la TEA, Prof. Mkenda ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Ufungaji wa maonyesho  hayo yaliyofanyika kwa wiki moja na kuongozwa na Kauli Mbiu, ‘Kuinua Ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Ajili ya Nguvu Kazi Mahari Tanzania”  alikutana na wanufaika wa  SDF wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Awali Prof. Mkenda alikutana na wanufaika wawili, Bi. Lisa Mkuyu na Bi. Witness Jacob ambao mara baada ya kupata mafunzo ya usindikaji wa vyakula kutoka kituo kinachotoa mafunzo cha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) cha jijini Dodoma mnamo mwaka 2021, walianzisha kampuni ya Roselyn Winnery ya jijini Dodoma, inayozalisha mvinyo aina Úgogon’na ‘Roselyn’.

Wanufaika wengine ni Bi. Sifa Lupasi aliyepata mafunzo SIDO Dodoma, ambaye sasa ni msindikaji wa bidhaa za chakula ikiwa ni pamoja na siagi ya karanga, asali, pilipili, unga wa lishe ambaye pia anatokea jijini Dodoma. Wanufaika wengine ni Yussufu Omari aliyepata mafunzo ya utengenezaji wa matofali ya kufungana yanayotumia udongo na saruji kidogo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Chala, mkoani Lindi; na Lamnyaki Lekoole aliyepata mafunzo ya Utalii na Huduma za Ukarimu katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mto wa Mbu ambaye kwa sasa anashughulika na utalii wakitamaduni huko Mtowa mbu, mkoni Arusha.

Mheshimiwa Waziri amewatia hamasa ya kuendela na jitihada za uzalishaji na kuangalia fursa nyingine ikiwa ni pamoja na kupata mikopo, ushauri wa kiufundi ili kukuza zaidi shughuli zao za uzalishaji.

Hadi sasa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi umetumia kiasi cha Sh Bilioni 12.3 kwa ajili ya kugharimia mafunzo ya kuwajengea vijana ujuzi na stadi za kazi. Hadi sasa, zaidi ya vijana elfu 34 nchi nzima wameshapata mafunzo kupitia ufadhili wa Mfuko wa kuendeleza ujuzi ambao unafadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Dunia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.