Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA Kuendelea Kushirikiana na Wadau Kuboresha Miun...

TEA Kuendelea Kushirikiana na Wadau Kuboresha Miundombinu ya Kujifunzia na Kufundishia

12 Oct, 2026
TEA Kuendelea Kushirikiana na Wadau Kuboresha Miundombinu ya Kujifunzia na Kufundishia

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kuboresha mazingira ya ujifunzaji nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza fursa za elimu bora na jumuishi kwa watoto na vijana.

Mnamo tarehe 14 Mei 2025, TEA na UNICEF walifanya kikao katika ofisi za TEA, Ilazo - Dodoma, kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu inayofadhiliwa na UNICEF kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ubora wa miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji nchini.

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, ambapo miradi 34 ya elimu ilijadiliwa, ikiwemo:

  • Utekelezaji wa miradi 7 chini ya Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya MfumoRrasmi (IPOSA),
  • Ujenzi wa maabara 52 katika mikoa ya Simiyu na Dodoma.

Ujumbe wa UNICEF Tanzania uliongozwa na Mwakilishi wake, Bi. Simone Vis, akiambatana na Dkt. Ayoub Kafyulilo (Mtaalamu wa Elimu) na Bw. Mohamed Hindi (Mhandisi wa Miradi ya Maendeleo).

Wadau hao walionesha kuridhishwa na namna TEA inavyosimamia miradi na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ili kuongeza tija ya uwekezaji katika sekta ya elimu kwa watoto wa Tanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kipesha aliishukuru UNICEF kwa kuendelea kuiamini TEA kama msimamizi wa miradi hiyo muhimu na kuahidi kuwa utekelezaji utafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora, ili kufungua fursa zaidi za ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Katika mwaka wa fedha 2023/2024, TEA kwa kushirikiana na UNICEF walitekeleza miradi 13 yenye thamani ya shilingi milioni 854. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya miradi 35 ilitekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.55, ikihusisha ujenzi na ukarabati wa maabara za sayansi, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika mikoa ya Tabora, Songwe na Kigoma