Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA yajipanga Kuboresha Miundombinu ya Mafunzo ya...

TEA yajipanga Kuboresha Miundombinu ya Mafunzo ya Amali

12 Oct, 2026
TEA yajipanga Kuboresha  Miundombinu ya Mafunzo ya Amali

Katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeidhinisha utekelezaji wa miradi 120 ya elimu yenye thamani ya Shilingi bilioni 11.5, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini. Miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha wanafunzi 38,803 kote nchini.

Katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha wanafunzi wa Tanzania wanapata stadi na ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 imetilia mkazo ujenzi wa miundombinu ya mafunzo ya amali.

Kiasi cha Shilingi bilioni 4.1 kimetengwa kwa ajili ya miradi ya mafunzo ya amali katika shule 30 zilizopo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Katavi, Kilimanjaro, Geita, Lindi, Iringa, Njombe, Manyara, Pwani, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tanga.

Fedha hizo zitatumika kugharamia ujenzi wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya amali katika maeneo mbalimbali, yakiwemo uzalishaji na afya ya wanyama, uzalishaji wa mazao, ujenzi, ufundi umeme, ubunifu wa mavazi, useremala, ufundi wa magari pamoja na michezo ya aina mbalimbali.