Uwanja mpya wa netiboli katika Shule ya Sekondari Mbeya umefungua fursa mpya kwa wanafunzi kukuza vipaji, nidhamu na kujiamini kupitia michezo.
Uboreshaji huo umewezeshwa na uwekezaji wa Shilingi milioni 66.65 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, uliotumika kujenga uwanja wa netiboli na kununua vifaa vya michezo, ikiwemo mipira, jezi na nyavu za magoli ya mpira wa miguu.
Miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika ni Neema Hamis Mkula, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Mkondo wa Amali ya Michezo, ambaye kipaji chake cha netiboli kimemwezesha kutunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Mwenye Nidhamu katika mashindano ya FEASSSA.
Neema anasema ndoto yake ni kuwa mchezaji wa kulipwa na baadaye kocha. Anaamini mazingira bora ya michezo shuleni yanaongeza nafasi ya wanafunzi kutambua na kukuza vipaji vyao.
Mwanafunzi mwingine, Pishon Enock, wa Kidato cha Tatu katika Mkondo wa Amali ya Michezo, anasema anatamani kuwa mchezaji wa mpira wa miguu wa kulipwa. Kwa mujibu wake, uwekezaji katika miundombinu na vifaa umeongeza hamasa kwa wanafunzi na hata wazazi kuhusu umuhimu wa Elimu ya Amali ya Michezo.
Mafanikio ya uwekezaji huo yanaonekana pia katika timu za shule, ambazo zimepiga hatua kutoka mashindano ya ndani hadi ngazi ya mkoa na taifa. Baadhi ya wanafunzi wamechaguliwa kujiunga na timu za kitaifa na kupata uzoefu kupitia mashindano ya FEASSSA.
Makamu Mkuu wa Shule, Bw. Christian Kyando, anasema maboresho hayo yameongeza hamasa, ambapo hata wanafunzi wa Mkondo wa Elimu ya Jumla wameanza kuvutiwa na Mkondo wa Amali ya Michezo.
Uwekezaji huo unaonesha namna TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa inavyoendelea kuimarisha Elimu ya Amali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kukuza vipaji na kupata ujuzi unaoweza kuwa msingi wa ajira na kujiajiri.
Kwa wanafunzi wa Mbeya Sekondari, uwanja huo si sehemu ya kucheza pekee, bali ni jukwaa la kukuza vipaji na kutengeneza fursa za maisha ya baadaye.
Shule ya Sekondari Katoro iliyopo mkoani Geita imepokea zaidi ya Shilingi...
Shule ya Sekondari Chief Sarwatt iliyopo Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, imepok...
Jumla ya shule 167 za sekondari nchini zinatekeleza mtaala wa Elimu ya Amali una...
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), kwa kushirikiana na Mamlaka ya E...
Miaka minne baada ya kupata mafunzo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), una...