Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA Yaimarisha Elimu ya Amali ya Michezo Katoro Se...

TEA Yaimarisha Elimu ya Amali ya Michezo Katoro Sekondari, WyEST Yasisitiza Ubora

01 Nov, 2026
TEA Yaimarisha Elimu ya Amali ya Michezo Katoro Sekondari, WyEST Yasisitiza Ubora

Shule ya Sekondari Katoro iliyopo mkoani Geita imepokea zaidi ya  Shilingi Milioni  207 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu na ununuzi wa vifaa vya michezo.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa uwanja huo, Msaidizi wa Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), Bi. Suzana Raphael, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ujenzi huo unazingatia viwango vya ubora vilivyowekwa ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuboresha elimu kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, amesema TEA itahakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Naye, Mwalimu wa Michezo wa shule hiyo, Mwl. Steven Johnson, ameishukuru Serikali kupitia TEA kwa ruzuku hiyo, akieleza kuwa uwanja huo utasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa eneo la kufanyia mazoezi na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Aidha, wanafunzi wameipongeza Serikali kwa kuanzisha mtaala wa Elimu ya Amali unaowawezesha kupata ujuzi wa vitendo na kujiandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira. Pia, wameiomba TEA kuwasaidia kupata vyumba maalumu vya kubadilishia nguo za michezo ili kuboresha mazingira ya kushiriki michezo shuleni.

Uwekezaji huu unaonesha jitihada za Serikali kupitia TEA katika kuimarisha Elimu ya Amali na kuweka mazingira bora ya kukuza vipaji vya wanafunzi nchini.