Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
Mtaala Wa Elimu Ya Amali Wanufaisha Shule 167 Nchi...

Mtaala Wa Elimu Ya Amali Wanufaisha Shule 167 Nchini, Dodoma Sekondari Ikiwa Miongoni Mwake

28 Oct, 2026
Mtaala Wa Elimu Ya Amali Wanufaisha Shule 167 Nchini, Dodoma Sekondari Ikiwa Miongoni Mwake

Jumla ya shule 167 za sekondari nchini zinatekeleza mtaala wa Elimu ya Amali unaolenga kuwapatia wanafunzi ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri, kujitegemea na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Abdul Maulid, alipotembelea Shule ya Sekondari Dodoma kukagua ujenzi wa karakana na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika fani ya upishi na uandaaji wa chakula (Food Production).

Mradi huo umefadhiliwa kwa ruzuku ya zaidi ya Shilingi milioni 198.03 kutoka Mfuko wa Elimu wa Taifa, unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambapo uwekezaji huo unalenga kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kutumia fursa zilizopo katika soko la ajira na kujiajiri.

“Tunashukuru Serikali kupitia TEA kwa kutoa takribani Shilingi bilioni 3.8 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa shule 16 kwa ajili ya ujenzi wa karakana na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule zinazotekeleza mtaala huu,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwalimu Francis Tumaini, amesema  upatikanaji wa vifaa vya mafunzo ya amali utaboresha utoaji wa mafunzo ya vitendo na hivyo kuwapatia wanafunzi ujuzi utakaowasaidia kujiajiri baada ya kuhitimu.

Ufadhili huo wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika vifaa na miundombinu ya mafunzo ya amali ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha Elimu ya Amali, kukuza ujuzi wa vitendo miongoni mwa wanafunzi na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi nchini.