Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA kwa kushirikiana na UNICEF yaleta mapinduzi ma...

TEA kwa kushirikiana na UNICEF yaleta mapinduzi masomo ya Sayansi mashuleni mkoani Songwe

26 Aug, 2026
TEA kwa kushirikiana na UNICEF yaleta mapinduzi masomo ya Sayansi mashuleni mkoani Songwe

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wameendelea kufanya mapinduzi makubwa katika kuinua ubora wa elimu nchini, hususan katika masomo ya sayansi. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano maalum yaliyosainiwa kati ya pande hizo mbili, yakilenga kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga na kukarabati maabara za sayansi katika shule mbalimbali za mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora.

Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe ni moja kati ya wilaya zilizonufaika na mapinduzi haya ambapo shule mbili zimenufaika na umaliziaji wa ujenzi wa maabara nne za Sayansi. Umaliziaji ujenzi na ukarabati wa maabara hizo unafanyika kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, ambapo takribani shilingi milioni 132 zimetumika.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Afisa Miradi kutoka TEA, Bi Atugonza David, alisema shule zilizonufaika ni Shule ya Sekondari Itumba, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 78.3 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya maabara, na Shule ya Sekondari Bupigu, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 54 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maabara mbili za Kemia na Fizikia.