Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA NA VETA KUTOA MAFUNZO YA UFUNDI KWA VIJANA 14,...

TEA NA VETA KUTOA MAFUNZO YA UFUNDI KWA VIJANA 14,000 WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

26 Aug, 2026
TEA NA VETA KUTOA MAFUNZO YA UFUNDI KWA VIJANA 14,000 WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

TEA NA VETA KUTOA MAFUNZO YA UFUNDI KWA VIJANA 14,000 WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameanza majadiliano ya ushirikiano yatakayowezesha vijana 14,000 wanaoishi katika mazingira magumu kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi kupitia Mpango wa Ufadhili (Bursary Scheme Scholarship).

Majadiliano hayo yamefanyika Agosti 6 jijini Dodoma katika kikao kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamis Chambega kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu kikihusisha Menejimenti ya VETA pamoja na timu inayotekeleza miradi ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) kutoka TEA.

Akizungumza wakati wa kikao hicho CPA Chambega amesema, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatekeleza Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ II), huku TEA ikiwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza programu hiyo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).

Mratibu wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi na Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi wa TEA Bw. Masozi Nyirenda amesema, programu hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita na inalenga kuwafikia vijana 14,000 wanaotoka katika mazingira magumu.

Ameongeza kuwa, ushirikiano na VETA utarahisisha kuwafikia walengwa na kuwapatia mafunzo husika kupitia mtandao mpana wa vyuo na vituo vya mafunzo ya ufundi stadi vilivyopo nchini.

“Ili kufanikisha lengo hili ni muhimu kushirikiana na taasisi zenye uwezo wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi. Tunaamini VETA ina uwezo wa kuwafikia vijana walengwa kupitia vituo vyake vilivyopo kote nchini,” alisema Bw. Nyirenda.

Alibainisha kuwa, wanufaika watapatiwa mafunzo ya muda mrefu yasiyozidi mwaka mmoja katika sekta 10 za kipaumbele ambazo ni kilimo na kilimo-biashara, utalii na huduma za ukarimu, ujenzi, nishati, TEHAMA, uchimbaji madini, mifugo na uvuvi, afya, usafirishaji na uchukuzi pamoja na uzalishaji viwandani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA Dkt. Abdallah Ngodu alisema, taasisi hiyo ina zaidi ya vyuo 80 na inasimamia zaidi ya vituo 904 vya mafunzo ya ufundi stadi nchini hivyo, ina uwezo wa kutoa mafunzo kwa wanufaika wote 14,000 wanaolengwa ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Aliongeza kuwa, Mpango Mkakati wa VETA umeweka kipaumbele katika kuongeza upatikanaji wa elimu kwa usawa kwa makundi maalumu ikiwemo vijana wanaotoka katika mazingira magumu na wanawake.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuharakisha maandalizi na hatimae kusaini mkataba wa ushirikiano utakaoweka msingi wa kuanza rasmi utekelezaji wa mpango huo.