Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
TEA na UNICEF Wawezesha Uendelezaji wa Masomo ya S...

TEA na UNICEF Wawezesha Uendelezaji wa Masomo ya STEM

08 Oct, 2026
TEA na UNICEF Wawezesha Uendelezaji wa Masomo ya STEM

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)- Tanzania chini ya ufadhili wa Serikali ya Canada, imewezesha ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa miundombinu ya maabara za sayansi katika shule za sekondari mikoa ya Kigoma, Songwe na Tabora.

Utekelezaji wa miradi hiyo umefanyika katika awamu mbili kuanzia Mwaka wa Fedha 2023/2024. Katika awamu ya kwanza, Shilingi milioni 344.2 zilitumika kwa ajili ya ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa maabara tisa (9), huku awamu ya pili iliyoanza mwaka 2024/2025 ikitumia Shilingi milioni 936.7 kufadhili vyumba 44 vya maabara katika shule 20.

Miradi hiyo imeleta matokeo chanya katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), ikiwemo kuongezeka kwa hamasa ya wanafunzi kuchagua mkondo wa sayansi.

Katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko, mkoani Kigoma, ujenzi wa maabara za Kemia, Biolojia na Fizikia umeboresha mazingira ya kujifunzia kwa vitendo. Makamu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Alex Lugaji Kagoma, amesema wanafunzi 58 waliohitimu Kidato cha Nne kwa mara ya kwanza mwaka 2024 walifanya vizuri, ambapo sita walipata Daraja la Kwanza, 42 Daraja la Pili na tisa Daraja la Tatu.

Aidha, Shule za Sekondari Itumba na Nkangamo mkoani Songwe zimeeleza kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi baada ya kuboreshwa kwa maabara. Hali kama hiyo imeonekana pia katika Shule ya Sekondari Kamagi mkoani Tabora, ambapo wanafunzi wameonesha hamasa zaidi kupitia Klabu ya STEM.

Miradi hiyo imewanufaisha pia wanafunzi katika shule za sekondari za Kigoma, Tabora na Songwe, zikiwemo Kashoza, Gwanumpu, Migezi, Rugenge, Busami, Nyamidaho, Nyakitonto, Mount Samba, Masanga, Dkt. J.P. Magufuli, Goweka, Langwa, Ngulu, Kizengi, Pangale, Usagali, Bupigu, Shiwinga na Ndugu.

Kwa ujumla, TEA kwa kushirikiana na UNICEF na Serikali ya Canada inalenga kuimarisha miundombinu ya STEM ili kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaowaandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia inayozidi kuongozwa na sayansi na teknolojia.