Masomo ya Amali ya Kilimo yanaendelea kuwa fursa muhimu kwa vijana kujenga ujuzi wa kujiajiri na hata kuajiri wengine, hasa kutokana na msisitizo wa mafunzo ya vitendo.
Mwalimu wa Amali ya Kilimo katika Shule ya Sekondari Uwemba, Bw. Christopher Mwenisongole, amesema wanafunzi wanaopata mafunzo hayo hujengewa uwezo wa kutumia ujuzi wao kuanzisha shughuli za kilimo baada ya kuhitimu.
Amesema ufadhili wa vifaa vya kilimo kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) umeongeza hamasa ya wanafunzi kushiriki katika mafunzo ya vitendo.
Irene Noela Mdoe, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, amesema alichagua Amali ya Kilimo kwa kuwa inachanganya nadharia na vitendo, jambo linalomsaidia kupata ujuzi kwa urahisi. Naye Abel Ayub Malongo, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu anayesomea uzalishaji wa mazao, amesema ana ndoto ya kuwa mkulima wa kisasa baada ya kuhitimu.
Mwenisongole amesema mwanzoni baadhi ya wazazi na jamii walikuwa na mashaka kuhusu masomo ya amali, lakini mtazamo umeanza kubadilika baada ya kuona manufaa yake. Shule pia imekuwa ikitoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo.
Makamu Mkuu wa Shule, Bw. Fadhili Mwangesongo, amesema mwaka jana shule ilipokea vifaa vya Amali ya Kilimo vyenye thamani ya Shilingi milioni 280, vikiwemo matrekta, greenhouse na vifaa vingine kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
Masomo ya Amali ya Kilimo yanaendelea kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Shule ya Sekondari Katoro iliyopo mkoani Geita imepokea zaidi ya Shilingi...
Shule ya Sekondari Chief Sarwatt iliyopo Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, imepok...
Jumla ya shule 167 za sekondari nchini zinatekeleza mtaala wa Elimu ya Amali una...
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), kwa kushirikiana na Mamlaka ya E...
Miaka minne baada ya kupata mafunzo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), una...